Je, huenda Kenya ikafuata mkondo huu mwaka 2017?

Hivi majuzi, tumeshuhudia mabadiliko ya kisiasa katika mataifa mbali mbali ulimwenguni. Kati ya mabadiliko haya ni kung'olewa mamlakani kwa viongozi ambao wamekuwa mamlakani kwa muda mrefu. Vile vile vyama vya kisiasa ambavyo vimekuwa katika upinzani vimeweza kutwaa hatamu za uongozi.

Hapa barani Afrika ni nadra sana kwa rais aliye mamlakani kushindwa katika uchaguzi hadi aamue yeye mwenyewe kutogombea kiti cha urais. Hili ni jambo ambalo linaonekana kuwakera watu wengi na kulingana na hali ilivyo kwa sasa, huenda mtindo huu wa kiimla ukakomeshwa na wapigaji kura.

Hapo mwaka 2015 Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha All Progressives Party (APC) aliweza kumng'atua mamlakani aliyekuwa rais Goodluck Jonathan wa People's Democratic Party(PDP). Chama cha PDP kimewahi kushinda chaguzi zote za urais nchini Nigeria kati ya mwaka 1999 na 2011. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa rais aliye mamlakani kushindwa katika uchaguzi nchini humo.

Wiki hii tumeshuhudia tukio sawa na hilo katika uchaguzi wa urais nchini Gambia kule Afrika Magharibi amabapo rais wa sasa Yahya Jammeh amekubali kushindwa na mpinzani wake Adama Barrow. Jammeh amekuwa mamlakani tangu mwaka 1994 wakati alipotwaa mamlaka baada ya mapinduzi ya kiserikali nchini Gambia. Licha ya kushutumiwa vikali na wananchi kwa uongozi wake mbaya, Jamme ameweza kukaa mamlakani kwa miaka 22 hadi uchaguzi wa hapo juzi ambapo Wagambia waliamua wanataka 'Gambia mpya". 

Huko Marekani, Rais mteule Donald Trump aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican aliweza kumshinda Hillary Clinton wa chama cha Democrats kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mapema mwezi uliopita. Hillary, ambaye aliungwa mkona na Rais Obama alitarajiwa na watu wengi duniani kushinda uchaguzi huo. Vyombo vya habari na makampuni ya utafiti yalitoa ripoti kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa Hillary kumshinda Trump kwenye uchaguzi huo. Hatimaye kinyume na matarajio ya wengi, Trump ambaye alitoa matamshi makali na yasiyopendeza wengi katika kampeni zake, alishinda uchaguzi huo huku akitoa ahadi ya kurejesha utukufu wa nchi hiyo.

Hapo jana Rais wa Angola Jose Dos Santos ambaye ameshutumiwa vikali na makundi yanayopinga ufisadi nchini humo alitangaza kutogombea urais kwenye uchaguzi ujao baada ya kutawala kwa takriban miaka 36 ijapokuwa hajatangaza sababu kamili ya kutogombea urais. Hata hivyo huenda shinikizo kutoka kwa baadhi ya wananchi na makundi yanayompinga ndiyo sababu kuu ya kuchukua hatua hiyo.

Hayo ni baadhi ya matukio tunayoyashuhudia wakati Kenya inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Katika historia ya nchi yetu hakuna rais ambaye ameweza kung'olewa mamlakani katika uchaguzi mkuu. Baadhi ya Wakenya wanasema kuwa serikali ya Jubilee, ambayo imeonekana kushindwa katika vita dhidi ya ufisadi, huenda ikang'atuliwa mamlakani mwaka ujao. Iwapo hilo litatendeka basi RaisUhuru Kenyatta atakuwa rais wa kwanza kushindwa katika uchaguzi mkuu hapa Kenya. Vile vile, atakuwa rais wa kwanza wa Kenya kutawala kwa kipindi kimoja cha miaka mitano pekee.