Maagizo mnayotoa yanaathiri maendeleo Maraga awaambia majaji

Na Suleiman Yeri
Siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kulalamikia ongezeko la maagizo yanayotolewa na mahakama, Jaji Mkuu David Maraga amesema maagizo hayo yanaathiri miradi ya maendeleo nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya siku nne ya majaji wa Mahakama Kuu mjini Naivasha, Maraga amewapa changamoto majaji kutathmini athari za maagizo wanayotoa, kwa vile mengi hurudisha nyuma na kukwamisha miradi ya maendeleo.
Wakati uo huo, Jaji Maraga amekiri kuwa ufisadi umekithiri katika idara ya mahakama na kuapa kulitatua tatizo hilo. Amedokeza kuwa asilimia kumi ya wafanyakazi, majaji na makarani walishiriki ufisadi, jambo lililoiharibia sifa idara hiyo.
Aidha amesema mbinu pekee ya kukabili ufisadi kuiimarisha Tume ya Utawala na Haki ili iwezeshwe kuchunguza visa hivyo. Hata hivyo amesema majaji wanaoshtumiwa kushiriki ufisadi watapewa nafasi ya kujitetea, huku akiwashauri kuungana naye katika kuukabili ufisadi.