Rais Kenyatta aendelea kuwasuta wasiotekeleza majukumu yao

Na Beatrice Maganga

Kwa siku ya pili leo hii, Rais Uhuru Kenyatta amezishtumu idara za serikali zisizozingatia utekelezaji wa majukumu hasa katika kukabili ufisadi na badala yake kulaumiana. Akizungumza mapema leo wakati wa halfa ya kumwapisha Jaji Mkuu mpya David Maraga, Rais amesema ni japo la kusikitisha kwa idara mbalimbali kukwepa kuwajibikia masuala mbalimbali na kuzilaumu nyingine.

Aidha ameitaka idara ya mahakama kuwajibika zaidi katika kuzishughulikia kesi mbalimbali zilizo mbele yake.

Akizungumza alasiri wakati wa halfa nyingine ya uzinduzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha, Rais vilevile amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kuwatambua maafisa wa serikali wasiowajibika kazini.

Wakati wa kikao na wanahabari jijini Nairobi, Kinara wa CORD Raila Odinga amesema serikali ya Jubilee ni kizingiti katika vita dhidi ya ufisadi na kwamba Rais Kenyatta ameshindwa kutekeleza majukumu yake. Anasema suluhu ya vita dhidi ya ufisadi ni wananchi kujitolea vilivyo kuukabili.

Hapo jana wakati wa kikao katika Ikulu, idara mbalimbali zikiwamo Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC, ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi DCI, maafisa wa Idara ya Mahakama, Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinett, kulikuwapo kulaumiana kwingi kuhusu suala kwamba ni idara gani imezembea katika vita dhidi ya ufisadi.