Washukiwa wa IS waachiliwa huru

Na Sophia Chinyezi

Wanaume wanne waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na kundi la linalojiita Dola la Kiislamu, IS wameachiliwa huru mapema leo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwafungulia mashtaka. Ali Musa, Hamisi Hakim, Yasin Ahmed na Mwinyi Mwabondo walikuwa wamezuiliwa rumande kwa siku saba.
Mkuu wa Mashtaka wa Serikali, Lydia Kigori aliiagiza mahakama kuwaachilia huru kwa kuwa polisi walishindwa kupata ushahidi wa kuwahusisha na kundi hilo. Hata hivyo Kigori alimshauri Hakimu Julius Nang'ea kuwaruhusu polisi kuendelea kumzuilia Mwambondo.
Amesema simu yake iliyowasilishwa kwa Kitengo cha Kukabili Uhalifu wa Mitandaoni inafanyiwa ukaguzi baada ya taarifa za kutiliwa shaka kupatikana humo. Washukiwa hao walikamatwa Oktoba saba katika Mahakama ya Mombasa baada ya kuhudhuria kikao cha kesi ya jamaa yao.