Magavana wakana kutoa matamshi ya uchochezi

Na Caren Omae

''Kauli zetu kuhusu uteuzi katika Chuo Kikuu cha Moi, hazikulenga kuwachochea wakazi kwa misingi ya kikabila''. Ndiyo kauli ya Gavana wa Uasin Gishu, Jackson Mandago alipokuwa akizungumza baada ya kuhojiwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi Nchini, DCI. Akiwahutubia wanahabari baada ya kuhojiwa, Gavana Mandago amesema malalamiko yao yanalenga kuhakikisha uteuzi katika vyuo vikuu nchini unafanyika kwa njia ya haki.

Hata hivyo amewalaumu baadhi ya wanahabari ambao amesema wanatoa taarifa za uongo kuhusu pingamizi za baadhi ya viongozi kuhusu uteuzi wa Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi, Laban Ayiro wiki jana.

Gavana Mandago, Mwenzake wa Marakwet Alex Tolgos na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walifika katika Makao Makuu hayo saa saba adhuhuri na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu. Mbali na madai hayo ya uchochezi, maafisa wa polisi wamesema kuna masuala mengine ambayo viongozi hao watahojiwa kuyahusu.

Wengine ambao wanatarajiwa kuhojiwa ni Mbunge wa Kesses James Bett, Alfred Keter wa Nandi Hills na Tiren Silas wa Moiben.

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi Joseph Nkaisery aliagiza viongozi hao kufika katika makao Makuu ya Upelelezi DCI kuhojiwa la sivyo wakamatwe.