Rais amwapisha Luteni Jenerali Robert Kariuki

Na Fredrick Muitiriri

 Huku usajili wa makurutu ukiendelea katika sehemu mbalimbali nchini, Rais Uhuru Kenyatta leo hii amemwapisha kamanda mpya wa Jeshi la Ardhini, Luteni Jenerali Robert Kariuki Kibochi. Katika sherehe iliyoandaliwa mapema leo katika Ikulu ya Nairobi, Rais amemtaka Kibochi kuitumikia nchi ya Kenya vilivyo huku akisema serikali yake iko tayari kukisaidia kikosi cha KDF kinapoendelea kutumika katika sehemu mbalimbali za bara la Afrika na kinapoilinda nchi hii.
Aidha ameipongeza KDF kwa kuwa mstari wa mbele kukabili ugaidi ambapo amesema hatua muhimu zimechukuliwa kuilinda Kenya dhidi ya magaidi. Ameongeza kuwa Kenya haitaafikia maendeleo iwapo hakuna usalama wa kutosha.
Waliohudhuria sherehe hiyo ni Waziri wa Ulinzi Raychelle Omamo, Katibu wake Kirimi Kaberia, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua na Mkuu wa Majeshi Jenerali Samsom Mwathethe.