Waislamu kote duniani wanasherehekea sherehe ya Idd-ul-Adha

Na, Suleiman Yeri

NAIROBI, KENYA, WAISLAMU kote duniani, Jumatatu hii wanasherehekea sherehe ya Idd-ul-Adha au sherehe ya kuchinja. Sherehe hii ni ya kuadhimisha kukamilika kwa ibada ya Hajj.

Kadhi Mkuu wa Kenya, Ahmed Muhdhar amesema Waislamu watatangamana katika misikiti mbalimbali nchini kwa swala ya asubuhi na baadaye kupata mlo ambapo waumini wakitakiwa kuchinja.

Muhdhar aidha amewataka Waislamu kutoa sadaka ya chakula hususan nyama ya mifugo kwa familia zisizojiweza.

Ibada ya Hajj ni nguzo ya tano katika dini ya Kiislamu na hufanywa kila mwaka katika Mji Mtakatifu wa Makkah nchini Saudi Arabia ambapo Waislamu kutoka mataifa mbalimbali husafiri hadi mji huo kutekeleza ibada hiyo.