Utendakazi wa Wizara ya ardhi kuchunguzwa

Na, Beatrice Maganga

Ili kuboresha utendakazi katika Wizara ya Ardhi, Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC imeanza mpango wa kufanya ukaguzi katiza wizara hiyo. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Halakhe Wako amesema ukaguzi huo unalenga kubainisha namna shughuli za ununuzi wa ardhi zimekuwa zikiendeshwa ili kukabili unyakuzi wa ardhi.
Wako aidha amesema ukaguzi huo utajumuisha utathmini wa utendakazi kwenye idara mbalimbali za wizara hiyo ili kuhakikisha zinazingatia sheria. Amesema hatua hiyo inajiri baada ya tume yake kupokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu ufisadi uliokithiri katika Wizara ya Ardhi.
Kwa upande wake Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Michael Mubea amesema ukaguzi huo utafanywa kwa uwazi hatua itakayowavutia wawekezaji mbalimbali.
Waziri wa Ardhi, Jacob Kaimenyi ameukumbatia mpango huo akisema utawapa imani wananchi wanaowekeza kwenye ardhi ili wasilaghaiwe wanaponunua ardhi.