Msemaji wa Serikali Awaonya Wanaowauzia Wanafunzi Petroli

Na, Suleiman Yeri
Kuna haja ya washikadau mbalimbali katika sekta ya elimu kushirikiana na kuandaa makongamano ya kujadiliana na wanafunzi kuhusu changamoto wanazopitia ili kukabili visa vya moto shuleni. Akizungumza katika kikao na wanahabari, Msemaji wa Serikali Erick Kiraithe amesema hatua hiyo itafanikisha mipango ya kukabili visa vya uteketezaji wa majengo shuleni.
Kiraithe amesema hafla hizo zitatoa fursa ya kuwatambua wanafunzi walio na ari ya kuendelea na masomo ili kuhakikisha wanapata haki ya kupata elimu.
Aidha amewaonya vikali wamiliki wa vituo vya mafuta wanaouza bidhaa hiyo bila kuzingatia sheria kwamba watachukuliwa hatua kali iwapo itabainika kwamba mafuta yaliyouzwa kwenye vituo hivyo yalitumika kuteketeza majengo shuleni. Vilevile amefichua kwamba uchuguzi unaendelea kuhusu madai kwamba baadhi ya visa hivyo vimechochewa na walimu wanaotaka kupandishwa vyeo au kuwa walimu wakuu.
Wakati uo huo, Kiraithe amesema serikali imesitisha shughuli ya kuwaondoa Wakenya nchini Sudan Kusini, baada ya serikali ya taifa hilo kusema imeweka mikakati ya kuimarisha amani.
Aidha amesema Wakenya wanaodai kuitishwa hongo na maafisa wa ubolozi wa taifa hili nchini humo kutumia mbinu mwafaka na kuwasilisha malalamiko yao ili hatua zichukuliwe.

 

Related Topics