×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Tumsifu Rais Uhuru Kenyatta kwa mema

County_Nairobi
 President Uhuru Kenyatta inspects a gun mounted on top of an Armoured Personnel Carrier

Wiki iliyopita, barua yangu kwa rais Uhuru Kenyatta, Joseph Nkaissery na ndugu Nelson Marwa ilipokelewa kwa hasira na wafuasi wa watatu hawa.

Baadhi ya jumbe nilizozipokea, kando na matusi, niliguswa hasa na hisia ya mwanadada mmoja. Dada huyu alinishauri niandike mazuri aliyoyafanya Uhuru Kenyatta, sio tu kuikashifu serikali kila wakati. Baada ya kumsikiza mwanadada huyu, nimeamua kuandika mambo mawili matatu mazuri aliyoyafanya rais, na ambayo kamwe yataishi akilini mwetu.

Ukabila

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa kiongozi wa kwanza kuweza kuthibiti kikamilifu serikali iliyojaa ukabila tangu tulipopata uhuru wetu miongo mitano iliyopita.

Bila shaka si rahisi kuwa nahodha wa taifa wakati vyeo na hata maamuzi muhimu serikalini hutolewa kwa misingi ya kikabila. Sumu hii ya ukabila imenyweshwa hadi watoto ambao sasa wanafahamu fika kuwa kabila hili ni bora kuliko ile. Kongole rais.

 Vijana na kazi

Rais alifanya kampeni kabambe wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, huku akiwaahidi vijana nafasi zaidi za kazi. Hii ndiyo ilikuwa kauli mbiu kuu wakati huo wa kampeni. Lakini hii imebakia kuwa ndoto. Vijana watapa vipi ajira huku wengi wao wakipokonywa maisha kwa mtutu wa bunduki? Ahadi ilikuwa kuwapa vijana ajira, sio kupunguza idadi yao kwa mauaji ya kiholela inayofanywa na maafisa wa polisi makachinja. Naam, nafasi za kazi zipo, shida ni kuwa vijana hawapo tena. 

Minghairi na haya, asante sana rais kwa kuwaandika ‘vijana chapakazi ‘ katika serikali yako. Nazungumzia vijana kama vile ndugu Henry Kosgey, Meja Jenerali Hussein Ali — wote hawa walikuwa washukiwa katika mahakama ya jinai kule Hague Uholanzi. Mashtaka yao yalifutiliwa mbali.

Nazungumzia vijana kama vile ndugu Francis Kimemia aliyekuwa mtumishi wa umma katika serikali ya Kibaki kando na kuhudumu pia katika serikali ya rais mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi. Wengine ni kamishna wa polisi Mathew Iteere, aliyekuwa msemaji wa polisi Eric Kiraithe, Chris Kirubi, Mark Bor, miongoni mwa wengine. Wote hawa ni vijana chipukizi waliomaliza chuo kikuu majuzi. Hakika serikali hii ina maono mazuri kwa vijana wa taifa hili.

Ufisadi

Ufisadi umekuwa kama mchezo wa kitaifa. Bila shaka serikali hii inahitaji medali ya dhahabu kwa kutoa mfano bora na hata kuvunja rekodi ya ufisadi. Kila kuchao wakenya wamekumbana na habari za ufisadi ambapo hel nyini za uma zimefujwa. Sio sakata ya NYS, Youth Fund, Eurobond, SGR na hata lile swala la ardhi ya shule la Lang’ata Primary. Ligi hii iko juu tu sana. Wakenya sasa wasubiri fainali ya kuuzwa kwa Kenya.

 Taifa polisi

Usalama wa taifa ni jambo muhimu. Kwa hivyo kuna kosa gani unapowasiliana na rafiki yako mpendwa rais Yoweri Kaguta Museveni toka Uganga kujifunza mbinu mpya za usalama. Bila shaka mbinu zake ngugu mseveni, hasa jinsi alivyokabiliana na ndugu Kizza Besigye hivi majuzi. Sote tulion jinsi polisi wa Uganda walivyomtwanga Besigye na kuvunja gari lake.

Wengi wanasema Besigye alimpiku ‘Man Sebbo’ katika uchaguzi uliopita, lakini hayo hayatuhusu sisi. Asante sana kwa kuongeza vifaa vya usalama badala ya chakula, elimu na maendeleo kwa wakenya. Kenya sasa ni kama Uganda.

Maendeleo

Hakika umeboresha Kenya na kutuweka katika ramani ya dunia. Kila mtoto Kenya sasa ana tarakilishi. Mambo ni dijitali sasa Kenya. Kila mara nikizuru shule za humu nchini naona watoto wakitumia tarakilishi ya karatasi ulioahidi. Hakika ulisema na ukaenda. Asante sana kwa kufanikisha Huduma Centre. Kuna tuhuma kuwa kabila bora inazidi kupokea vitambulisho huku wale kutoka katika maeneo ya upinzani wakikosa vitambulisho. Hilo bila shaka litashughulikiwa.

Maendeleo yako sasa yamefanya wanyama kuishi na binadamu kwa raha mustarehe. Je, wakumbuka kuna simba sita waliopitia maeneo ya Lang’ata kuwasalimia wakenya? Majuzi pia naarifiwa mmoja alionekana katika barabara ya Mobasa akijaribu kuwaamkua wakenya. Hii ni maendeleo hasa kwa wanyama wote walio madarakani.

Usalama

Bila shaka usalama unaaza na wewe (mkenya), sio serikali. Tumepoteza wakenya wengi kupitia vitendo vya kigaidi. Wana mpeketoni walipoteza watu wanaokisiwa kuwa 95, 64 waliuwawa katika jumba la Westgate huku 147 wakiaga kule Garissa. Visa hivi viligonga vichwa vya habari kote kote. Tumepoteza wapendwa wetu, uchungu unaozidishwa pale mataifa ya kigeni wanapo waonya raia wake kutozuru Kenya.

 Ziara

Kenya lazimaijulikane kote duniani. Hivyo kunaubaya gani rais akizuru Hakika kama kuna mtalii bora duniani ni wewe kiongozi. Ziara za kuuza sera na maendeleo ya Kenya kwa misingi ya kupaa angani kila kukicha bila ya matunda ya safari zako. Hakika umevunja rekodi zaidi hata ya watalii walio na mazoea ya kuzuru mataifa ya nje. Umebakisha tu kueka bendera ya Kenya mwezini sawia na wamarekani. Leo hii wakenya wamelazimika katika mitandao kukutunuku jina la kiongozi mtalii.

Nina mengi yakukusifia kama wanavyotaka wachache waliofungika na ukabila na walio wagumu kutetea haki ya wakenya kwa sababu ni zamu ya kabila zao kunyonya damu ya kabila zingine. Ningelipenda kukusifia zaidi lakini muda hauniruhusu kwa leo. Hakika wakenya watakuzawadia mwaka wa 2017 kwa yale yote mazuri uliowafanyia kinyume na katiba ya Kenya. Tuzo kwa mpigo unalo 2017! Ashakum si matusi.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles