×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Serikali lazima ikome kuwakandamiza vijana wanaojieleza

News

Mwamko mpya miongoni mwa vijana yaonekana kuwatia tumbo joto wana-jubilee huku uchaguzi wa mwaka wa 2017 ukikaribia.

Matamshi ya baadhi ya makanisa hivi majuzi yakiwashawishi wafuasi wao kutoipigia serikali kura katika uchaguzi ujao baada ya kuona hila za serikali pale ilipojaribu kudhibiti jinsi huduma za kidini zinavyoendeshwa.

Leo, joto la kisiasa linazidi kutanda sasa huku vijana wakishika usukani kuikosoa serikali iliyoonekana kuwajali vijana wakati wa kampeini pekee.

Sasa jeshi la mageuzi ya tatu kupitia mitandao almaaruf kwa lugha ya kimombo Kenyans on twitter (KOT), bloggers na wanahabari fulani wameanza kulengwa.

Tumeshuhudia kukamatwa kwa wana maoni mitandaoni wakiwemo Robert Alai, Dikembe Disemba, Cyprian Nyakundi, waandishi wa habari kufutwa kazi kwa sababu ya kukashifu utenda kazi wa Serikali.

Mfano mzuri ukiwa kule kufutwa kazi kwa mhariri Galava aliyefanya kazi na shirika la Nation Media Group. Na hivi majuzi mwanahabari Yassin Juma alikamatwa kwa tuhuma zisizo eleweka.

Badala ya kuwakamata wezi wa Euro-bond, Anglo-leasing, NYS na Chicken Gate, serikali imeamua kuwawinda wanaolalama kutohudumiwa na serikali walioichagua kuwaondoa katika janga la matatizo.

Majuzi afisa wawili walisimamishwa kazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema aliwaona wakipokea hongo barabarani huko Mombasa katika mojawapo ya ziara yake. Kama ni kweli walipokea hongo basi ni sharti sheria zifuatwe. Wakamatwe wafikishwe mahakamani na rais aje kotini kutoa ushahidi wake kama aliyeshuhudia. Hii ya kufuta watu kiholela pasi na kusikizwa yatukumbusha enzi za nyuma.

Kenya imekuwa taifa yakutawaliwa kwa vitisho na kuhadaiwa kwa wanaouliza maswali. Polisi nao wanakuza chuki miongoni mwa wakenya kwa kupendelea upande fulani.

Watetezi wa haki za binadamu wanazidi kuzimwa, magari ya usalama yatanunuliwa kwa wingi si kutulinda sisi bali kutumika mwaka 2017 dhidi ya watakaopinga matokeo ya kibepari. Dhulma hizi zote ni njama ya kuandaa maandalizi kabambe ya kuchukua uongozi kwa mabavu na kujifanya watakatifu katika zoezi hilo.

Kwa sasa njia iliyobakia ya kipekee ni kumaliza kila sauti inayopinga dhulma na kuuliza maswali nyeti. Sauti iliyochoshwa na uongozi tasa wa vijijini na wa kibepari. Uongozi wa kiimla wa ni lazima yetu yenu hatujui. Kukamatwa kwa wana-blogu na kufutwa kwa wanahabari sio suluhu bali inatupa motisha ya kutaka kuuliza zaidi.

Serikali inafaa ifahamu kuwa katika karne ya sasa hakuna anayeogopa kufutwa kazi kwa kusema ukweli. Hizo enzi zilipitwa na wakati. Kwa matunda ya uhuru kupatikana ni sharti kila mkenya ainuke na kuuliza maswali pasi na kuogopa wizara ya ulinzi wa siasa na miungu midogo midogo iliyogeuza kenya kuwa soko la viazi karai.

Kukamatwa tutakamatwa, lakini domo hatutafyata tukiona mabaya dhidi ya wakenya wenzetu.

Jubilee imevuruga mzinga wa nyuki na ni sharti ijiandae kudonwa na vijana waliojaa hamaki ya mageuzi. Leo hii polisi wakenya wameshindwa kuwawinda wahalifu, wezi wa mali ya umma na badala yake kuamua kuwakamata wasio na hatia eti kwa sababu ya kusema kweli.

Enyi wanafiki, anzeni kujenga jela za kisasa, ongezeni vituo vya polisi maana itabidi mtukamate sote kwa kudai haki yetu.

Tukamateni Mombasa kisha mtuhukumu kiambu kama mlivyomfanyia Yassin Juma. Badala ya kumpeleka katika mahakama ya Makadara karibu na eneo aliloshikwa mliamua kumpeleka katika mahakama ya kaunti ya Kiambu kumfanyia unyama. Mlichosahau ni kuwa Mungu hana chama wala hashirikiani na wanafiki kuendeleza sera zao bovu. Sasa mmekosa lakumfanyia Yassin na badala yake kuanza kujadili ishara ya kidole chake.

Lo! Naona safari hii mtatukata vidole maana tutaendelea kutoa shahada hadi kiama kwamba hakuna apasaye kubudiwa ila Allah na Muhammad ni mtume wake. Lazima mfahamuni wazi kuwa Kenya imekomaa na wakenya wamekomaa zaidi.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles