×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Ahmed Darwesh: Dunia ni mapito, tusitembee kwa kujinaki, bali tuwe wastaarabu

News

Mwezi wa Disemba ndio huo unaanza kutupungia mkono wa buriani na ni wazi kuwa ifikapo juma lijalo wenye kusherehekea Krismasi watakuwa wamejihami kwa kila aina ya maandalizi na mapochopocho yanayoafiki pato la mtu na jinsi mtu anavyotaka kuisherekea sikukuu yenyewe. Lakini je ushawahi kujiuliza wanaosherehekea hutumia mbinu zipi katika kuadhimisha na kuisherehekea Krismasi?

Kinaya kikuu ni kwamba wengi huwa na ubadhirifu na utumizi mbaya wa pesa na kufanya mambo yasiyopendeza katika dini na hata katika jamii. Nikisema hivi namaanisha kuwa itakuwa si vyema ifikapo wakati wa Krismasi upike vyakula vingi, na kuishia kuvisoza mapipani kwa mtazamo kuwa unataka kujitangaza kwamba wewe ni bingwa wa mabingwa katika fani ya maandalizi huku ubavuni mwako kukiwa na majirani kadhaa ambao hawajatia tonge mdomoni mwao kutokana na hali ngumu za kimaisha.

Wito wangu mkuu ni kuwa unapojiandaa kuchinja au kupika mapochopocho wafikirie zaidi wale ambao hawana mbele wala nyuma kwani hata wao wana hamu ya kufurahia kama mlimwengu yeyote yule. Zaidi ni kuwa huu ni wakati muafaka wa kuzuru makao ya watoto mayatima na kuwahusisha katika kufurahia baraka mzomzo ulizokirimiwa na maulana.

Huu sio wakati wa kujishebedua na kuonyesha jinsi unavyoweza kuchafua meza kwa kila aina ya pombe na ulevi wa kupindukia. Ni hulka ya Wakenya kwamba tunasifika sana kwa Pombe,Siasa na Wanawake. Nawasuta wale wote ambao hunywa wee, mpaka ukadhani mtu amefunga tangi chini ya kitovu.

Namaanisha walevi mbwa ambao hufikia upeo wa kuokotwa mitaroni siku ya pili, na si ajabu ukawakuta wakiwa wamejikojolea au hata kubwabwaja maneno ya kukosa heshima mbele ya halaiki ya watu. Aibu! Watakaofanya hivyo wakati huu, fedheha kwenu. Mumetuchosha.

Mwezi wa Disemba ni wakati ambao ajali za barabarani hukithiri kwa kiasi kikubwa. Madereva hasa wa magari ya umma nawaomba muwe makini na watulivu katika kuwasafirisha abiria kutoka pembe moja ya nchi hadi nyengine.

Mukiwa na haraka ya kutaka kubeba abiria na kuwajaza hadi pomoni pamoja na kutaka kubeba safari nyingi zaidi, mujue mutajiponza kutokana na mwendo wenu wa kasi. Haraka haraka haina baraka, walisema wavyele. Mukijitia hamnazo basi si ajabu kuyaona magari yenu yamepiga pindu na mengine kuvurujika nyang’anyang’a kwa kutozingatia sheria na kanuni za usalama wa barabarani. Tunawataka nyinyi nyote mukiwa wazima wa afya ili tuuone mwaka mpya pamoja.

La msingi, tunapokaribia kuumaliza mwaka tumshukuru Maulana kwa dhati ya nafsi zetu kwa kutufikisha hapa tulipofika.

Wengi walitamani kuwa nasi,lakini maradhi, ajali na hata majaaliwa yamewafifiza na kuwaweka mbali na macho ya walimwengu. Wangapi tuliokuwa nao jana na juzi hii leo wamekwenda mbele za haki. Seuze mimi na wewe ambaye hatujui siku yetu itafika lini?

Dunia mapito, sote tu wapita njia, tusitembee juu ya ardhi kwa hashuo na kujinaki bali tuwe wastaarabu, wapole na watulivu hapo ndipo tutaufaidi utamu wa maisha.

Lakini tukifanya mambo kwa papara tutazijutia nafsi zetu,ndiposa nakokoteza umuhimu wa kupima maji na unga. Tusije tukala shendea. Lamsingi ni kuwa kila ulitendalo wakati huu lifanye kwa kiasi na kujikisi. Mambo na kipimo ati, kwani mno ikizidi mno huwa ni mno. Mujienjoy! Kama alivyopenda kusema Mzee Kibaki.

Hii ndio ilikuwa nakala ya mwisho aliyowasilishwa mwendazake Darwesh siku moja kabla ya kuaga dunia. Jamii ya The Nairobian inazidi kuomboleza na familia, marafiki na wafanyikazi wote wa shirika la The Standard Group.Tunaomba Mola amweke pema penye wema. Daru, kama alivyojulikana na marafiki, alikuwa Mhariri Mkuu na msoma habari wa KTN Leo.

Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.Buriani Kaka Daru.

Marehemu Darwesh alikua mwandishi wa nakala ya Falsafa za Busara katika gazeti hili

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles